Mashabiki wa mashetani wekundu wasema,”Glazers out.”

Mashabiki shakiki wa Manchester United wanazidi kugoma na kuwataka Glazers kuondoka katika klabu hiyo.Glazers ndio waliochukua usukani wa kumiliki na kuiongoza klabu ya Manchester United tangu mwaka wa 2005.

Image
Mashabiki wa Manchester United wakigoma ili wamiliki wa klabu hiyo waondoke.Hii ni kabla ya mechi yao na Liverpool kuanza.

Takriban wiki mbili zilizopita aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hii,Woodward, alijiondoa uongozini baada ya presha kutoka kwa mashabiki wa Manchester United.Hii inajiri baada ya viongozi hao kujiunga na ligi ya “European Super League” iliyoanzishwa na rais wa Real Madrid ,Florentino Perez.Mashabiki walidai kuwa hawakuhusishwa kwenye uamuzi huo na kuongezea kuwa ligi hiyo itamaliza ladha na ushindani wa haki kwenye kandanda barani Ulaya.

Glazers bado hawajatoa kauli yao kuhusiana na mgomo wa mashabiki wanaowataka kuondoka.

‘European Super League’ ilikuwa nini haswa na mbona ilifeli?Nani walitaka iwe?

Kumekuwa na vita vya maneno na kutoelewana baina ya washikadau wa UEFA,FIFA na waanzilishi wa ‘European Super League’.Ligi hii ya Super League imefanya mashabiki wa kandanda kumekemeana na kukashifu vilabu vyote vikubwa vilivyosaini kondrati na ‘Super League.’

Lakini,European Super League ni nini?Mbona ‘ European Super League ilifeli?’Ni akina nani walitaka Super League iwe na kwa nini?

Image
Florentino Perez

European Super League ilikuwa iwe mfumo mpya wa kandanda tofauti kidogo na klabu bingwa bara Ulaya.Kulingana na Florentino Perez ambaye inaaminika ndiye mshirika mkuu wa ligi hii,anaamini kwamba UCL inachosha mashabiki na haina msisimko hata kidogo isipokuwa inapofikia hatua ya robo fainali.Anasema wanastahili kuanzisha mbinu mpya ya kuvutia mashabiki kwani wengi wao wanapenda mechi zinazohusu timu kubwa zenye mashabiki na historia kubwa.

Perez alikuwa ajumuishe timu kumi na tano katika ligi ya ‘European Super League’ zenye historia nzuri ya ufanisi kutoka ; Uingereza (timu sita ),Uhispania (timu tatu),Ujerumani (timu tatu),Italia (timu tatu).Baadaye,wangejumuisha timu nyingine tano ambazo zinafanya vizuri kwenye ligi.Kungekuwa na vikundi viwili A na B ambavyo vingejumuisha timu kumi kila kundi.Timu tatu bora zinafuzu moja kwa moja mpaka raundi ya robo fainali kisha timu zilizomaliza nambari nne na tano katika kila kundi zinacheza mechi mbili na kuamua timu mbili zitakazojiunga na sita zilizo katika robo fainali.Fainali ingekuwa inachezwa wikendi huku mechi za makundi zikichezwa katikati ya wiki.

Perez anaamini kwamba kuanzishwa kwa ‘European Super League’ kungesaidia vilabu viweze kujikwamua katika lindi la madeni.Anasema kwamba msimu huu Real Madrid watakuwa na hasara ya yuro milioni mia moja themanini.Aliendelea kusisitiza kwamba UEFA imejaa wafisadi ambao wanafinyilia timu kubwa huku wao wakibaki na donge nono la pesa.Alisema hakuna mtu hata mmoja anayejua mshahara wa rais wa UEFA,Ceferin.Lengo lake kuu la kuanzisha ligi hii ilikuwa kukwamua timu katika madeni,kuleta msisimko na mfumo mpya katika kandanda manake UCL haivutii watu kama lilivyokuwa hapo mwanzoni.

Image
Perez

Florentino Perez ambaye pia ni rasi wa Real Madrid anasema kwamba vilabu vilikuwa tayari vimesaini mkataba na ligi hiyo.Kujiondoa kwao si kwa sababu mashabiki waligoma bali ni kwa sababu waliogopa UEFA na FIFA.Perez anasema kwamba mashabiki wa Chelsea waliokuwa wakigoma walikuwa arubaini pekee na hawakugoma kwa hiari bali ni kuletwa waliletwa na wanaopinga kuanzishwa kwa ‘European Super League’.Vilabu viliogopa kufukuzwa kwenye UCL na ligi zao za nyumbani.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Christiano Ronaldo kurudi Real Madrid alisema kwamba haiwezekani na wanaosukuma ajenda hiyo ni wandani wa Ronaldo.Alisema kwamba hakuna vilabu vikubwa vitakavyosaini wachezaji wenye tajiriba kubwa manake takriban vilabu vyote vimefilisika na kujaa madeni.Alisema kwamba mashabiki waliotaka Mbappe na/au Haaland watakuwa na subira mpaka msimu ujao kwani haiwezekani kuwasaini kwa sasa.Alisisitiza kwamba Real Madrid ina wachezaji wachanga wazuri kama Rodrygo na Asensio na watauza baadhi ya wachezaji ili kudumia pesa walizo nazo.Perez alisema kwamba hatima ya Sergio Ramos haijulikani kwani yeye ndiye atakayeamua iwapo atakubali kupunguza mshahara na kubakia pale Santiago Barnabeau.

Image
Ronaldo na Perez

Inaaminika kwamba aliyekuwa rais wa Barcelona,Bartomeu, ndiye aliyekuwa akisukuma ligi hiyo iwe manake yeye ndiye angekuwa rais wa kwanza wa ‘European Super League’.Pia,Agnelli wa Juventus alikuwa mmoja wa vigogo wa ligi hiyo.Perez alisema kuwa mpango huo wa European Super League umesimamishwa kwa muda na anasema kwamba yote yanatokana na UEFA kutowasikiliza.Perez ambaye ana miaka 72,anakiri kwamba amekuwa akilala kwa kuchelewa na kuamka mapema kwa miaka mitatu iliyota ili kuweka mikakati kabambe ya ligi hii.Hata hivyo,anasema kwamba vilabu havijajitoa kabisa na kuwa watarejelea mpango huu usoni.

Image
Bartomeau (kushoto) na Perez (Kulia)

PSG kutawazwa mabingwa wa klabu bingwa bara Ulaya?

Kulingana na habari iliyotolewa na UEFA kuhusu timu zinazojiunga na ligi kuu ya Ulaya (European Super League),PSG ya Ufaransa huenda ikatawazwa mabingwa wa dimba la klabu bingwa bara Ulaya.UEFA ilisema kwamba timu zote zinazoshiriki ligi hiyo zitatimuliwa katika mechi za ligi za nyumbani na mechi zote za klabu bingwa bara Ulaya.

Image
Neymar ,fowadi wa PSG

Hii ina maana kwamba,iwapo UEFA watashikilia uamuzi huo basi Chelsea,Real Madrid na Bayern hazitashiriki katika nusu fainali ya kombe la klabu bingwa bara Ulaya.Bayern walikuwa wamekataa mwaliko wa kucheza ligi hiyo lakini walibadilisha uamuzi huo na huenda Leipzig na Porto pia wakajumuika na ligi hiyo kuu ya Ulaya.

Katika mechi ya Uropa,Roma na Villarreal huenda zikacheza fainali ya kombe hilo iwapo Manchester United na Arsenal zitatimuliwa na UEFA.

Mwenyekiti wa Ligi kuu ya Ulaya Florentino Perez amesema iwapo wachezaji watakaoshiriki ligi hiyo hawataruhusiwa kucheza katika kombe la dunia,ataanzisha kombe lake la dunia yeye mwenyewe na washikadau wengine.

“Timu zitakazoshiriki kwenye SuperLeague zitatimuliwa kwenye ligi”

Perez ambaye ni rais wa timu ya Real Madrid pamoja na washikadau wengine kwenye ngazi za juu za kandanda wameibua gumzo katika hatima ya kandanda Ulaya.Hii ni baada ya kuamua kuja na mpango wa kejenga ” ligi kuu” ambayo itashirikisha timu bora Ulaya haswa katika zile ligi tano bora zinazotambulika zaidi.

Uingereza inahitajika kutoa timu tano au sita bora,Uhisapania na Italia timu tatu.Ligi ya Ufaransa na Ujerumani hazikujumuishwa haswa baada ya Borrussia Dortmund na Bayern Munich kukataa mwaliko wa kushiriki katika ligi hiyo.

Mechi za ligi hiyo zinapangwa kwamba zitakuwa zikichezwa katikati ya wiki na zitajumuisha makundi mawili yenye timu kumi kila upande.Timu nne bora katika kila kikundi zitafuzu katika mkondo mwingine na hatimaye timu mbili bora kucheza fainali wikendi.Pia,waratibu wa “superleague ” wanasema kwamba kutakuwa na kushushwa daraja kwa timu zitakazokuwa na matokeo mabovu.

Shirikisho la kandanda la Uingereza (FA) limetoa msimamo wao unaopinga vikali kuwepo kwa “Superleague”.Wanasema kwamba ligi hiyo haitakuwa na ushindani wa haki na kuwa itaharibu kandanda.

Borris Johson ambaye ni waziri mkuu wa Uingereza pia amepinga kuanzishwa kwa ligi hiyo na kuombwa vilabu vinavyohusishwa kushirikisha mashabiki wao katika maamuzi.

Timu zozote zitakazokubali mwaliko huo zitapokea kitita cha Yuro milioni 425.

Baadhi ya akaunti za kandanda katika mtandao wa Twitter zinakiri kwamba zimekataa kuchukua pesa kutoka kwa washikadau wanaotaka akaunti hizo ziegemee upande wa wazo hilo la “Superleagu”.Wanasema kwamba huko ni kuharibu utamu wa kandanda na kwamba timu nyingi zitafilisika zikishiriki michuano hiyo.

UEFA imekashifu swala hili vikali na kusema kuwa zitapinga ligi hiyo vikali kortini.Aidha,imesema kuwa timu zitakazoshiriki katika ligi hiyo hazitaweza kucheza mechi za ligi za nyumbani na mechi ngingine za kimataifa.Pia,wachezaji hawataweza kuwakilisha timu zao za kitaifa hata kidogo.

Wakenya waishutumu serikali kwa kukandamiza mwanachi wa kawaida

Jumamosi mwendo wa saa mbili unusu hivi usiku ,polisi walieka vizuizi katika barabara tofauti na kusababisha msongamano wa magari.Barabara ya Thika ilionekana kuwa kitovu cha hasira kwa wakenya kwa kuwa msongamano ulikuwa mkubwa ajabu na ni kana kwamba wanapolisi walitaka watu walale barabarani kwenye magari yao.Walitaka iwe funzo kwa wanaoenda kinyume na sheria za serikali za kudhibiti msambao wa virusi vya Corona wakati wa kafyu inayoanza saa mbili Usiku.

Image
Thika Road

Wakenya kwenye mitandao ya kijamii waliikashifu hatua ile na kusema kuwa haisadii chochote bali ni kuwakandamiza wananchi wa kawaida.Wengi wanasema kuwa ni vigumu mtu kutafuta riziki yake na kuweza kufika nyumbani mapema kabla ya muda ya kafyu kwa kuwa magari ni machache kwenye stendi ilhali abiria ni wengi kupita kiasi.

Kanda za video zilisambaa katika mtandao wa Twitter ambazo zilivunja watu nyoyo.Akina mama wengine walikuwa na watoto wachanga huku wengine hali zao za kiafya zikiwa si nzuri.Inasemekana kuwa polisi walichukua funguo za baadhi ya magari yaliyokuwa karibu na kizuizi kilichokuwa katika barabara ya Thika jambo lililosababisha msongamano huo.

Image
Thika Road

Hata hivyo,kuna baadhi ya wakenya waliohisi kuwa hatua hiyo ilikuwa sawa ili watu wafuate taratibu za serikali.Upande mwingine,sehemu kubwa ya wakenya walisema kuwa huo ni ufashisti wa serikali dhidi ya mwananchi wa kawaida ambaye anafanya vibarua vidogo kama kazi ya “bebabeba” na wengine kuuza nguo za mtumba ili kujaribu kukimu mahitaji yao ya lila siku.

Swali ibuka ni je,serikali itasikiza kilio cha wananchi na kusukuma saa za kafyu mpaka mwendo wa saa nne usiku au italifumbia swala hili macho?

Wajua Messi ana mataji mengi kuliko miaka yake?

Ushindi wa Barcelona dhidi ya Athletic Club ulimsaidia Messi kutwaa taji lake la saba la Copa del rey katika fainali kumi alizoshiriki.Mataji mengine ambayo Messi ameshinda ni;

La liga mara 10

Spanish Supercup mara 8

Kombe la klabu bingwa bara Ulaya mara 4

Fifa club world cup mara 3

Uefa supercup mara 3

Lionel messi ana miaka 33 na ameshinda mataji thelathini na matano akiichezea klabu ya Barcelona .

Image
Messi na kombe la copa del rey

Lionel Messi atamba dhidi ya Athletic Club na kuandikisha rekodi nyingine

Lionel Messi ameandikisha rekodi na kuvunja iliyokuwa imeshikiliwa na Gerd muller na Fernando Peyroteo waliokuwa wachezaji wa pekee kupiga magoli thelathini na zaidi (30+) katika misimu kumi na miwili mtawalia.Messi alipiga magoli mawili dhidi ya Athletic Club katika fainali ya Copa del rey na kufikisha mabao thelathini na zaidi katika misimu kumi na mitatu mtawalia.

Image

Kando na hayo,Lionel Messi ameshiriki mechi 80 za copa del rey na kupiga magoli 56 na kupakua mengine 33. Kwa jumla amechangia magoli themanini na tisa katika mechi themanini za kombe hili.Rekodi iliyokuwa imeshikiliwa na Telmo zarra ya kuwa na mabao mengi katika fainali ya kombe hili ilivunjwa na messi.Telmo alikuwa na magoli manane.Lionel Messi alipachika magoli mawili dhidi ya Athletic Club na kumfikisha hadi magoli tisa katika fainali kumi za copa del rey.

Image

Mzawa huyu wa Argentina pia amecheza fainali 43 katika tasnia yake ya kandanda na kufunga kucheka na nyavu mara 31 na kupakua mengine 13.Kwa jumla amechangia magoli 44 katika mechi 43 alizoshiriki.

Slavia Prague yakabwa koo na Arsenal : Arsenal kukutana na aliyekuwa kocha wao Unai Emery katika hatua ya semifainali

Baada ya kutoka sare ya goli moja kwa moja katika mkondo wa kwanza,Arsenal walijikomboa kwa kuisakama Slavia Prague magoli manne kwa sufuri katika mkondo wa pili.

Image

Arsenal walianza mechi kwa kasi na kupiga goli la kwanza lakini Smithe Rowe akawa ameotea.Dakika za kuhesabu baadaye,Nicolas Pepe alifunga goli safi na kuwapa Arsenal uongozi kabla ya Lacazette kupiga la pili kupitia mkwaju wa penalti.Magoli hayo yalifungwa katika dakika ya 18 na 21.

Image
Lacazette akishangilia goli

Bukayo Saka hakuachwa nyuma kwenye karamu ya magoli kwa kucheka na nyavu katika dakika ya 24, na kuipa Arsenal uongozi wa magoli matatu kwa nunge katika kipindi cha kwanza.Bukayo Saka amecheza mechi 15 za Europa na kupiga magoli manne na kupakua mengine manane.

Image

Japokuwa kipindi cha pili kilikuwa butu,Arsenal walipata goli jingine kupitia sentafowadi wao Lacazette katika dakika ya sabini na saba ,77.Lacazette ana jumla ya magoli kumi na moja katika robo fainali ya dimba hili la Uropa.Ni Radamel Falcao aliye na magoli mengi zaidi katika hatua hii ya Uropa kuliko Lacazette:ana magoli kumi na sita.

Katika mechi nyingine za Uropa:

Manchester United waliichabanga Granada ya Uhispania magoli mawili kwa nunge.Goli la kwanza lilipigwa na Cavani huku Parejo akijigunga la pili na kuizawadi United ushindi wa 2-0.

Villareal nao walibwaga Dinamo zagreb magoli mawili kwa moja huku Roma na Ajax wakitoka sare ya goli moja kwa moja.

Mechi za semifainali:

Villarreal vs Arsenal

Roma vs Manchester United

Pep akosa maarifa dhidi ya wachezaji kumi wa Leeds United

Manchester city waliialika Leeds United ugani Etihad katika ligi kuu ya Uingereza.Huku City wakizidi kukaribia taji la EPL,leeds United walikuwa wanasaka nafasi ya kumaliza kumi bora katika msimamo wa ligi.

Manchester city walitawala umiliki wa mechi na kuwa na mashuti mengi kuliko Leeds United lakini hawakuwa na bahati ya kupata goli.Dallas alipata shuti la kwanza la Leeds United na kupata goli la kwanza katika dakika ya 35.Dakika kumi na moja baadaye kabla ya mapumziko, Cooper alilishwa kadi nyekundu kwa kumchezea Gabriel Jesus ngware.Kipindi cha kwanza leeds walikuwa na shuti moja pekee huku Manchester City wakiwa na mashuti kumi na moja.Aidha,City walikuwa na umiliki wa asilimia 63 huku leeds wakimiliki asilimia 37 ya mchezo.

Image

Leeds United walirudi mchezoni katika kipindi cha pili wakiwa na ari ya kuzuia mashambulizi ya Manchester city.Fowadi wa City,Ferran Torres aliwasawazishia Manchester city katika dakika ya 76 baada ya kupakuliwa pasi na Bernado Silva.

Image
Ferran Torres

Leeds United walizidi kujituma mchezoni na kushambulia kwa wakati mmoja.Dallas alipata nafasi nyingine ya kuweza kuwapa Leeds United ushindi lakini Ederson akapiga mlazo na kumnyima goli hilo.Vijana wa Bielsa walipata nafasi ya mwisho katika dakika ya 90 na kipindi hiki Dallas hakupoteza nafasi ile.Alimpiga Ederson nyebwe na mpira ukaingia kimiani na kufanya matokeo kuwa 1-2.Leeds United sasa wamo katika nafasi ya kumi huku Arsenal wakishuka hadi nafasi ya kumi na moja.

Image
Leeds wakishangilia goli

Kinyang’anyiro cha kubeba taji la EPL huenda kikachukua mkondo mpya ingawa Manchester United wako alama kumi na nne nyuma ya viongozi Manchester City.

Mguu mmoja wa Chelsea umeingia Semi fainali

Chelsea iliandikisha ushindi muhimu zaidi katika mkondo wa kwanza wa UCL dhidi ya Porto kutoka Ureno.Mechi yenyewe haikuwa na kasi na Porto walionekana kucheza mchezo mzuri wakilinganishwa na wageni wao,Chelsea.

Chelsea walipata goli lao la kwanza kupitia Mason Mount.Hilo lilikuwa shuti la kwanza la Chelsea katika mechi hii na lilizalisha bao hilo huku Jorginho akipakua pasi ile.Hilo lilikuwa goli la kwanza la mason mount katika dimba hili la ucl katika mechi 15 alizocheza.

Image

Porto walizidi kujikakamua katika kipindi cha pili huku Mendy akilazimika kuokoa mpira kutoka kwa Marega ambao nusura uingie nyavuni.Christian Pulisic naye alidhani amepata bao la pili lakini moira ukagonga chuma.

Ben Chilwell ndiye aliyeihakikishia Chelsea ushindi katika dakika ya 85 kwa kumchenga golikipa na kuutia mpira kimiani.Porto itakuwa na kibarua kigumu katika mkondo wa pili kwani watahitajika kupiga magoli matatu kwa nunge (3-0) iwapo watataka kujikatia tiketi ya nusu fainali.Kama Mason Mount tu,hilo lilikuwa goli la kwanza la chilwell katika kipute hiki cha UCL.

Image
Chelsea

Rekodi zaandikishwa huku Bayern wakifunzwa kandanda na PSG

Bayern Munich walisamu amri dhidi ya PSG kwa kukubali kurindimwa magoli matatu kwa mawili (2-3) ugani Alianz Arena.

Psg walianza mechi kwa kasi baada ya Neymar kumtilia Mbappe pasi na kupata goli katika dakika ya tatu.

Image

Bayern walitawala mechi na pasi zao kuonana lakini mashambulizi yao yalikuwa butu.Wachezaji wao tegemeo kama vile Gnabry na R.Lewandowlski hawakuwepo kutokana na majeraha.Nahodha wa PSG,Marquinhos alipiga bao la pili katika dakika ya 28 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Neymar.

Image
Marquinhos akifunga goli

Bayern Munich walitoa makucha yao na Chupo Moting akapiga goli la kwanza kwa wenyeji katika dakika ya 37.Katika kipindi cha pili,Thomas Muller alisawazisha mambo kuwa 2-2 katika dakika ya 60.

Image
Muller

Hata hivyo,furaha yao iligeuzwa huzuni baada ya Mbappe kupiga goli la tatu na la ushindi katika dakika ya 68 baada ya kupokea pasi mufti kutoka kwa Di Maria.

Katika mechi hii,Neymar aliandikisha rekodi nyingine kuwa mchezaji wa pekee wa Brazil kuwa na magoli mengi na kupakua (assist) mabao mengi katika dimba hili la vilabu bingwa bara Ulaya (UCL).Aitha,ndiye mchezaji aliyepakua mabao mengi tangu mwaka wa 2012/2014.Amepakua mabao 26 huku Christiano Ronaldo akifuatia kwa ukaribu kwa 23.

Image

Mbappe naye ameweza kuchangia na kufunga magoli 42 katika mechi 43 alizocheza UCL.Kati ya hizo,amefunga magoli 27 na kupakua mengine 15.Ibainike kuwa ana miaka 22 pekee.Aitha,ameweza kumpiku Robin Van Persie na Griezman katika mabao ya UCL kwani wote wana magoli 26 kila mmoja wao huku yeye akiwa na mabao 27: Sawia na Luis suarez na mario Gomez.

Image

Thomas Muller naye aliandikisha goli lake la 48 katika mechi 123 za UCL.Mabao hayo yanampeleka katika nafasi sawa na Shevchenko na Zlatan Ibrahimovic.

Zaidi ya hayo,Bayern wameweza kupiga magoli 68 katika mechi za mwisho 20 walizoshiriki.

Manchester City yapata ushindi mkonde dhidi ya Dortmund

Dortmund walikaribishwa ugani Etihad na vijana wa Pep Guardiola katika robo fainali ya kombe la klabu bingwa bara Ulaya.Manchester city walijikakamua kuzima makali ya Dortmund ambayo yaliwatatiza kutokana na ubora wa washambulizi wao.City waliandikisha goli la kwanza katika dakika ya 19 baada ya De Bruyne kutiliwa pasi nzuri na Mahrez.

Dortmund walidhani kuwa wamepata goli la kusawazisha kupitia Bellingham lakini VAR ikafutilia mbali goli hilo kwa sababu,ni kama Bellingham alimchezea Ederson ngware kabla ya kufunga.Wengi wa wachambuzi wa kandanda wanaamini kuwa goli hilo lingefaa kusimama.

Image
Bellingham dhidi ya Ederson

Kipindi cha pili Dortmund walizidi kuvizia lango la city huku wenyeji wakifanya kila jitihada kuzuia magoli.Haaland alipiga pasi iliyounganishwa na Reus na kupata goli la kusawazisha katika dakika ya 84.

Image
Reus

Haaland sasa ana mabao kumi na amepakua mengine mawili katika mechi saba alizoshiriki katika kipute hiki.

City walionekana kuwa na kiu ya kuponyoka na ushindi.Phil Foden aliikonga kiu hiyo ya ushindi katika dakika za lala salama (90) baada ya kutiliwa pasi tamu na De bruyne.

Image
Foden

Manchester city wataenda katika mkondo wa pili ugenini Signal Eduna Park wakiwa na uongozi mkonde wa 2-1.Yeyote anaweza kufuzu katika semi fainali kwani ushindi huu ni finyu sana.Iwapo Dortmund watashinda kwa goli moja katika mkondo wa pili,basi watafuzu semi fainali kwa ajili ya goli la ugenini.Iwapo,kutakuwa na sare yoyote,basi city watafuzu kwa wingi wa magoli.

Vinicious Junior aizamisha Liverpool

Liverpool walipigwa katika mkondo wa kwanza wa robo fainali ya dimba la klabu bingwa bara ulaya na Real madrid.Vinicious Junior alikuwa na mchezo mzuri na wakati huo huo akimdhalilisha Trent Alexander arnold na kumfanya asutwe mitandaoni na mashabiki wa kandanda.

Viniciors alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 27 kisha Asensio akapiga la pili katika dakika ya 36.

Image
Vinicious akishangilia goli

Liverpool walikuwa na mchezo mbovu manake hawakuweza hata kupiga shuti lolote lililolenga golini katika kipindi cha kwanza .Hata hivyo,kipindi cha pili walitawala mechi na kuianza vizuri.Mohammed Salah aliipa Liverpool matumaini kwa kupiga goli katika dakika ya 55.

Image

Real Madrid walipiga kaunta nzuri ambayo ilizalisha goli la tatu muhimu katika dakika ya 65 kupitia Vinicious Junior.Hii ni mara ya kwanza kwa mchezaji huyu wa Brazil kuweza kupiga magoli mawili katika mechi moja tangu aanze kucheza soka ya kulipwa.

Ingawa Liverpool walipoteza kwa jumla ya magoli matatu kwa moja kule Uhispania,bado kuna tumaini kuwa wanaweza kufuzu katika semi fainali.Wanachohitaji ni kushinda magoli mawili kwa nunge (2-0) katika mkondo wa pili kule Anfield.

Harry Kane ni moto wa kuotewa mbali

Harry Kane anazidi kuibuka kuwa miongoni mwa washambulizi matata ulimwenguni katika kila mechi anayoicheza.Tangu msimu wa 2014/2015 hadi msimu huu wa 2020/2021,Hary Kane ameweza kupiga magoli thelathini au zaidi katika mechi zote za taifa na klabu isipokuwa msimu wa 2018/2019 ambao alipiga magoli 27.

Image

Msimu huu Kane anaongoza katika orodha ya wafungaji bora katika ligi ya Uingereza kwa magoli kumi na tisa.Anafuatiwa karibu na Mohammed Salah na Bruno Fernandez ambao wana magoli 18 na 16 mtawalia.Kane pia anaongoza kwa kuwa mchezaji aliyepakua pasi nyingi zilizozalisha mabao ,(13 assists) katika mechi 28 pekee za ligi.

Hakuna mchezaji mwengine katika ligi tano bora za Ulaya aliye changia magoli mengi kuliko Kane isipokuwa Robert Lewandowlski.Kane amechangia mabao 32 ya ligi huku Robert Lewandowlski akiwa na 41.Lionel Messi anawafuata kwa mchango wa magoli 31.

Katika mechi zote alizoshiriki tukijumuisha msimu huu,Kane amechangia magoli 49 katika mechi 49 alizochezea Tottenham na Uingereza.

Image

Harry kane anafukuzia rekodi ya kuwa mfungaji bora katika ligi ya Uingereza.Sasa hivi,anaorodheshwa wa sita kwa magoli 163,goli moja chini ya Robbie Fowler.Fowler amecheza mechi 141 zaidi ya Harry Kane.

Image
Robbie Fowler

Kane ameweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyefunga magoli mengi ugenini katika ligi ya Uingereza.Ametinga magoli 80 katika mechi mia moja na ishirini.

Katika tasnia yake ya kadanda ya mechi za ligi ya uingereza ,Kane amecheza mechi 238 na kupachika magoli 162 na kupakua mengine 33.

Image

Newcastle yalazimisha sare dhidi ya Tottenham Hotspur

Newcastle United walitoka sare ya magoli mawili kwa mawili na Tottenham Hotspur katika uga wa St James Park.Newcastle walifungua karamu ya mabao kupitia mshambulizi wao Joelinton katika dakika ya 20.

Harry Kane ambaye amekuwa katika fomu nzuri msimu huu alisawazisha goli hilo baada ya kupata pasi mufti kutoka kwa Lo Celso:Katika dakika ya 30.Dakika nne baadaye Harry Kane alipiga goli jingine alipotiliwa pasi murua kutoka kwa Ndombele.

Image
Harry Kane

Kipindi cha pili Tottenham walionekana kuwa butu kwani dakika za kwanza ishirini hawakuwa wamepiga shuti lolote katika lango la Newcastle.Ingawa walipata nafasi kadhaa baadaye,walishindwa kuzitumia na Newcastle wakawaadhibu katika dakika za lala salama.Willock aliwapa Newcastle alama moja muhimu sana kwa kufunga goli la kulazimisha sare katika dakika ya 85.